Mlinzi wa Meja Jenerali aliyejeruhiwa kwa risasi Dar akamatwa - Mazingira FM

Mazingira Fm Live

Breaking News

Wednesday, 13 September 2017

Mlinzi wa Meja Jenerali aliyejeruhiwa kwa risasi Dar akamatwa

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linawashikilia watu wawili akiwemo mlinzi wa Suma JKT na mhudumu wa benki ya NBC tawi la Tangibovu ambao wanatuhumiwa katika tukio la kujeruhiwa kwa risasi Meja Jenerali Mstaafu wa Jeshi la Wananchi Tanzania(JWTZ), Vincent  Mritaba.

Kamanda wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa amesema leo Jumatano kuwa Septemba 11 mwaka huu saa 11 jioni maeneo ya Tegeta Masaiti jeshi hilo lilipata taarifa ya Mritaba kuvamiwa na watu wawili wasiojulikana ambao walimjeruhi na kumpiga risasi ya begani, tumnoni na kwenye paja la mkono wa kulia huku wakimpora kiasi cha Sh5 milioni.

Amesema tukio hilo lilitokea baada ya mstaafu huyo kutoka kuchukua fedha hizo katika benki ya NBC tawi la Tangibovu akiwa kwenye gari lake ya Volkswagen Amarok.

Mambosasa amesema alipofika nyumbani kwake alipiga honi na kufunguliwa geti na mlinzi wake Godfrey Gasper.

Amesema geti lilipofunguliwa pikipiki ilisimama hapo getini na watu wawili waliokuwa wamevaa helment walishuka na kulifuata gari huku wakiwa na silaha aina ya bastola ndipo walishambulia upande wa kulia wa dereva na katika kioo cha mbele.

"Huku wakimwamuru ashuke ambapo risasi zilimjeruhi maeneo ya begani, tumboni na kwenye paja la mkono wa kulia na kutokomea kusikojulikana kwa kutumia pikipiki waliokuja nayo," amesema Mambosasa.

Mambosasa amesema cha kushangaza wakati mlinzi huyo anaenda kufungua geti silaha yake aina ya shotgun yenye namba TZCAR9644 aliiacha kwenye kibanda cha ulinzi huku ikiwa chini ya kitanda.

Amesema baadaye watuhumiwa walimwambia akimbie katika eneo hilo na yeye alitii amri hiyo na kwenda mbali na tukio hilo jambo ambalo linatia shaka.

"Ninavyojua askari wa Suma JKT anapewa mafunzo ya ukakamavu haiwezekani uache silaha chini ya kitanda unakwenda kufungua geti kitu ambacho sikubaliani nacho,"amesema

Amesema walipofuatilia mawasiliano ya mmoja wa wahudumu wa benki hiyo walibaini kuwa alikuwa anapanga mipango na watu mbalimbali wanaokwenda katika benki hiyo. Hivyo msako mkali unaendelea ili kuwabaini watuhumiwa waliohusika katika tukio la kujeruhi kwa risasi afande huyo.

Pia alizungumzia kuvunjwa kwa ofisi ya wakili ya Prime Attoneys akieleza kuwa wanaendelea na msako mkali ili kuwabaini waliohusika katika tukio hilo na watakapokamatwa watachukuliwa hatua za kisheria.

No comments:

Post a Comment