KIKAO cha wazazi katika shule ya sekondari
Kibara, iliyoko wilayani Bunda, mkoani Mara, kimepitisha maazimio kadhaa, ili
shule hiyo iendelee kutoa elimu bora kwa wanafunzi na kufanya vizuri kitaaluma
mara kwa mara.
Katika taarifa ya kikao hicho iliyotolewa
jana kwa vyombo vya habari na mkurugenzi wa shule hiyo Mtamwega Mgaywa amesema
kuwa kikao cha wazazi wa wanafuzi wanaosoma katika shule hiyo kimeketi desema
22 mwaka huu.
Amesema kuwa katika kikao hicho wazazi
wamezungumzia changamoto mbalimbali zinazoikabili shule hiyo, ili kuzirekebisha
na kuleta ufanisi zaidi, ili wanafunzi waendelee kupata elimu iliyo bora zaidi.
Mgaywa ameyataja baadhi ya maazimio ya wazazi
hao kuwa ni pamoja na mtu yeyote kutokuifunga shule hiyo, bila kushirikisha
wazazi wenye watoto na bodi ya shule na kwamba pia shule hiyo isiingiliwe na
mtu yeyote, wanasiasa wala maslahi ya kisiasa, na badala yake ibaki na masuala
ya elimu tu.
Ameyataja maazimio mengine kuwa ni migogoro
yoyote ipelekwe kwenye bodi ya shule na ikishindikana ipelekwe kwenye vyombo
vya sheria, ambapo jingine ni kama kuna madai yoyote yafuate utaratibu wa kazi
na siyo vinginevyo.
Katika kikao hicho pia wazazi wameazimia mkuu
wa shule hiyo afanye marekebisho ya ajira na azingatie mwenye sifa ya taaluma
ya elimu, ikiwa ni pamoja na kuboresha uongozi wa shule na kwamba pia
kitafanyika kikao cha wazazi na bodi hapo Januari 3, mwakani, ili kuweka
mikakati mingine ya kimaendeleo zaidi.
No comments:
Post a Comment