Mkurugenzi Muwasa aingia matatizoni....Ni Baada ya Waziri Mkuu Kumtupa TAKUKURU - Mazingira FM

Mazingira Fm Live

Breaking News

Saturday, 20 January 2018

Mkurugenzi Muwasa aingia matatizoni....Ni Baada ya Waziri Mkuu Kumtupa TAKUKURU

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameamuru Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Mara kumkamata na kumuhoji Mkurugenzi Mtendani wa Mamlaka ya Maji Musoma (Muwasa) Gantala Said kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za mradi wa maji Bunda.

Mbali na mkurugenzi huyo pia ameiagiza Takukuru imuhoji mkurugenzi wa kampuni ya ujenzi ya Nyakirang'anyi, Mahuza Mumay ambaye ndiye mkandarasi anajenga mradi huo unaotoa maji kutoka Ziwa Victoria kwenye eneo la Nyabehu hadi Bunda mjini.

Waziri Mkuu amefikia uamuzi huo jana Ijumaa jioni baada ya mkurugenzi huyo kushindwa kueleza kitu kilichosababisha mradi wa maji Bunda kutokamilika  pamoja na Serikali kutoa fedha nyingi.

Akizungumza katika kikao maalumu cha kujadili changamoto za utekelezaji wa miradi ya maji mkoani Mara, alichokiitisha mjini Bunda, Waziri Mkuu alisema alimua kuitisha kikao hicho baada ya kutoridhishwa na utekelezwaji wa miradi hiyo hususan inayosimamiwa na Muwasa.

Alisema kwa sasa Serikali inatekeleza kampeni ya Rais John Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani. Kampeni hiyo  inayolenga kuwaondolea wananchi tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama, hivyo itawachukulia hatua wote watakaokwamisha miradi ya maji.

Waziri Mkuu alisema malengo ya kampeni hiyo ni kuwafikishia wananchi huduma ya maji safi na salama katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao.

Pia Majaliwa aliagiza kupitiwa upya kwa mradi huo   kwa sababu hafurahishwi na ujenzi wake.

“Kama mkurugenzi wa Muwasa anasema mradi umekamilika kwa asilimia 98 sasa kwa nini wananchi walalamikie kukosa huduma hiyo.”

Alisema mkurugenzi huyo amekuwa akimlipa mkandarasi fedha kabla ya kufanya kazi ambapo hadi sasa tayari mkandarasi anayenga mradi huo ameshalipwa zaidi ya Sh 7 bilioni na mradi haujakamilika na wananchi wanaendelea kutumia maji ambayo siyo salama.

Waziri Mkuu alisema viongozi hao wahojiwe na wakibainika kuhusika na ubadhilifuu wa fedha za mradi huo, wachukuliwe hatua kali za kisheria.

“Serikali imedhamiria kuimarisha huduma za maji, hivyo hatuhitaji mtu atakayeenda kinyume na mpango huo.”

Mradi wa kupeleka maji kwenye mji wa Bunda maji kutoka Ziwa Victoria katika eneo la Nyabeho ulisanifiwa mwaka 2006 na ulikuwa unatekelezwa kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha za maendeleo.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima aliagiza kufungwa na ofisi za Muwasa na kuwataka wafanyakazi wa mamlaka hiyo kutoruhusiwa kuingia ofisini hadi hapo uchunguzi utakapokamilika.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamalaka ya Maji Musoma, Mhandisi Said Gantala (kushoto) akitoka kwenye ukumbi wa Balili Rock Resort  mjini Bunda baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuamuru kuwa akamatwe na ahojiwe na TAKUKURU Januari 19, 2018.Kulia ni Kamanda wa TAKUKURU  wa mkoa wa Mara, Alex Kuhanda.

No comments:

Post a Comment