Mwanakwaya Afariki Kanisani Baada ya Kutoa Sadaka - Mazingira FM

Mazingira Fm Live

Breaking News

Wednesday, 24 January 2018

Mwanakwaya Afariki Kanisani Baada ya Kutoa Sadaka

Mwanakwaya wa kwaya ya Kanisa Katoliki la Mtakatifu Secilia, Kigango cha Muze Parokia ya Zimba Jimbo la Sumbawanga, Flora Nandi (25), ameanguka na kufariki dunia muda mfupi baada ya kutoa sadaka ya shukrani akiwa kanisani.

Tukio hilo la kifo cha mwanakwaya huyo wa kwaya ya Mtakatifu Secilia lilitokea Jumapili saa 4 asubuhi wakati wa idada ya kwanza.

Akisimulia tukio hilo Katekista wa kanisa aliyekuwa akiongoza ibada hiyo, Philipo Lupadasi, alisema kuwa wanakwaya wakiwa wanaimba na marehemu muda mfupi baada ya Lupadasi kutoka kutoa sadaka ya shukrani na kuendelea kuimba.

Alisema ghafla aliangua chini hali iliyozua mtafaruku na kusababisha ibada kusimama kwa muda mfupi, hali iliyowafanya wanakwaya wenzake kumnyanyua na kumtoa nje ya kanisa, ili pate hewa wakiamini kuwa amepoteza fahamu.

Katekista huyo alisema baada ya kumpepea kwa muda wanakwaya wenzake waliona Flora hapati fahamu, hali iliyowalazimu kumkimbiza katika zahanati ya kijiji cha Muze kwa ajili ya matibabu.

Alisema baada ya kufikishwa katika zahanati hiyo alipokewa na wahudumu wa afya na baada ya kufanyiwa uchunguzi ilibainika kuwa walimpeleka katika zahanati akiwa ameshafariki dunia.

Baada ya kupewa taarifa ya kifo hicho wanakwaya hao waliangua vilio hali iliyosababisha washindwe kurudi kanisani kuimba katika ibada ya pili, hivyo kuuchukua mwili wa marehemu na kuupeleka nyumbani kwake.

Katekista huyo alifafanua kuwa Flora wakati anafariki dunia alikuwa na ujauzito wa miezi mitano.

Kwa upande wake mwalimu wa kwaya ya Mtakatifu Cecilia, Aloyce Mwandanje, alisema kuwa kifo cha mwanakwaya mwenzao kimewaachia majonzi makubwa, ingawa ni mapenzi ya Mungu.

Alisema mwili wa marehemu ulizikwa Jumatatu katika makaburi ya Kijiji cha Muze.

No comments:

Post a Comment