Aliyekuwa Kaimu Kamishna wa Madini, Ally Bondo Samaje amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu mashtaka mawili ya matumizi mabaya ya madaraka.
Samaje amefikishwa katika mahakamani hiyo jijini Dar es Salaam Februari 9, 2018.
Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambna na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Victoria Nongwa kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo, April 9, 2013 na Juni 21, 2013 Makao makuu ya Wizara ya Nishati na Madini.
Amesema akiwa Kaimu Kamishna wa Madini, alitumia madaraka yake vibaya kwa kushindwa kuishauri Bodi ya Madini katika utoaji wa leseni ya madini ya Graphite na Marble kwa Kampuni ya Tanzaniteone Mining Limited na State Mining Corporation.
Katika shtaka la pili, April 16, 2013 makao Makuu ya Wizara ya Nishati iliyopo wilaya ya Ilala, akiwa Kaimu Kamishna wa Madini na Katibu wa Bodi ya Ushauri wa Madini kutoka wizarani, alitumia vibaya madaraka yake kwa kutoa maelekezo kwa msaidizi wake John Nayopa kuandaa leseni za madini ya Graphite and Marble, bila kufuata sheria ya madini.
Mshtakiwa yupo nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili na mmojawapo kusaini bondi ya Sh 50milioni.
Pia mshtakiwa hatakiwi kusafiri nje ya nchi bila kibali cha Mahakama.
No comments:
Post a Comment