Na Godfrey Kahango, Mwananchi
Mahakama ya Hakimu Mkazi-Mbeya imewaachia kwa dhamana washtakiwa Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi na Katibu wa Chadema Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Emmanuel Masonga katika kesi inayowakabili ya kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli.
Sugu na Masonga wamekaa mahabusu kwa muda wa siku 24 baada ya kunyimwa dhamana na mahakama hiyo kutokana na hoja za upande wa Jamhuri.
Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Michael Mteite amewaachia kwa dhamana wawili baada ya Wakili upande w utetezi, Peter Kibatala kuiambia mahakama hiyo kwamba imeshafunga ushahidi wake ambapo mashahidi sita walitoa ushahidi wao.
Mawakili wa pande zote mbili walikubaliana kwamba Februari 19 watawasilisha majumuisho ya shauri hilo mahakamani hapo.
Hakimu Mteite amekubaliana na hoja hiyo ya mawakili na kusema hukumu ya kesi hiyo itatolewa Februari 26 mwaka huu.
"Washtakiwa wote wanaachiwa kwa dhamana, na kila mmoja atajidhamini mwenyewe kwa hati ya dhamana ya maneno ya Sh5 milioni kwa kila mmoja.
Chanzo- Mwananchi
No comments:
Post a Comment