Kibiti yatenga bil 5.3 ujenzi wa makao makuu ya wilaya - Mazingira FM

Mazingira Fm Live

Breaking News

Sunday, 11 February 2018

Kibiti yatenga bil 5.3 ujenzi wa makao makuu ya wilaya



HALMASHAURI ya wilaya ya Kibiti, Mkoani Pwani, imetenga kiasi cha sh. bil 5.3 kwa ajili ya ujenzi wa makao makuu ya wilaya hiyo yanayojengwa na SUMA JKT, ujenzi ambao upo hatua ya kuchimba msingi.
Aidha imetenga sh. bil. 2.4 kwa ujenzi wa daraja kubwa la kuunganisha eneo la Mbuchi na Mbwera lenye urefu wa mita kumi.
Akizungumzia baadhi ya utekelezaji wa masuala ya miundombinu,maji,chakula na mifugo, makamu mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Yusuph Mbinda ,alisema pia wametenga mil.969.1, zitakazotumika katika ujenzi wa daraja la Mwake lenye urefu wa mita 40 .
Mwenyekiti huyo ,alisema miradi yote ipo katika hatua za mwanzo za ujenzi na unaendelea.
Pamoja na hayo,alisema wakandarasi wanafanya utafiti wa vyanzo vya uchimbaji visima katika vijiji mbalimbali lengo likiwa kuwaondolea kero ya ukosefu wa maji wananchi,mradi utakaogharimu mil.319.2.##
Mbinda alitaja ,vijiji vinavyotarajia kunufaika na mpango huo kuwa ni Nyamisati, Mtunda, Mchungu, Mahege na Kivinja A.
Vingine ni Ruma, Mlanzi, Mjawa, Nyakinyo, Kilula, Tambwe, Bumba Msoro na Miwaga/Ngulakula.
Mbinda alielezea, kupitia utekelezaji huo unaosimamiwa na ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), baada ya kukamilika kwa mradi huo utaendana na upatikanaji wa maji.
Alisema hatua hiyo itasaidia kuongeza idadi ya watumiaji wa huduma hiyo kutoka wateja 24,581 sawa na asilimia 65 mpaka kufikia 122,648 sawa na asilimia 85.
Katika hatua nyingine ,Mbinda alisema hali ya chakula ni nzuri, na kwamba hiyo inatokana na wananchi kujikita zaidi katika kilimo cha kisasa cha mazao ya chakula na biashara ikiwemo mpunga, mahindi, ufuta, muhogo na korosho.
“Pamoja na changamoto ya soko la zao kuu la biashara, upande wa korosho kutokana na ubora wake, bado tunaimani kupitia ilani ya Chama Cha Mapinduzi tutaweza kuwasaidia wananchi wetu kujikwamua kupitia kilimo hicho,” alieleza.
Mwenyekiti huyo alisema, mwaka wa 2017/2018 Kibiti pekee imezalisha tani 5,430,667 kutoka tani 3,713,163 mwaka 2016 sawa na ongezeko la asilimia 46.25 ya uzalishaji wa zao hilo.
Akizungumzia suala la mifugo, alisema wilaya inakadiriwa kuwa na ng’ombe 44,739, mbuzi 5,368 na kondoo 3,517 huku vijiji 19 kati ya 58 vimetenga maeneo ya malisho baada ya mpango wa matumizi bora ya ardhi, jumla ya hekta 21,984.79 zimetengwa kwa ajili ya malisho .
Mbinda alisema ,halmashauri hiyo inaendelea na zoezi la upigaji chapa mifugo .

No comments:

Post a Comment