Mwaka mmoja jela kwa wizi - Mazingira FM

Mazingira Fm Live

Breaking News

Saturday, 17 February 2018

Mwaka mmoja jela kwa wizi



MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wilaya ya Manyoni,Mkoani Singida imemuhukumu Musa Haruna (47) mkazi wa Kijiji cha Mtimkavu,kata ya Itigi,wilayani Manyoni kutumikia adhabu ya mwaka mmoja jela baada ya kumtia hatiani kwa kosa la wizi wa bomba tatu za chuma zenye thamani ya shilingi milioni mbili laki mbili elfu na themanini mali ya Wakala wa barabara Tanzania(TANROADS).

Mahakama hiyo ilimtia hatiani mshitakiwa baada ya kukiri na kukubaliana na hoja zote za mashtaka,ikiewemo kukamatwa na bomba tatu za chuma zilizopatikana kwa njia isiyo halali,kufikishwa polisi na kufikishwa Mahakamani.

Awali Mwendesha Mashtaka wa serikali,Geofrey Luhanga alidai kwamba sept,23,mwaka jana saa 1;30 usiku katika eneo la mtaa wa Majengo,mjini Itigi,Musa Haruna alikutwa na bomba za chuma tatu zenye thamani ya shilingi milioni 2 na laki mbili elfu na themanini zilizopatikana kwa njia isiyo halali mali ya Wakala wa barabara Tanzania (TANROADS).

Aidha Luhanga alidai pia kwamba hakuna kumbukumbu za makosa ya nyuma hivyo aliiomba Mahakama hiyo kwamba adhabu zinazotolewa na Mahakama kwa makosa ya aina hiyo ziwe kali ili ziwe fundisho kwa watu wengine wenye nia ya kutenda kosa kama hilo.

Kwa mujibu wa Mwendesha Mashtaka huyo wa serikali mabomba hayo yalikuwa yakitumika kwa alama mbali mbali za barabarani na makosa hayo yamefanywa kwa makusudi na mshitakiwa huyo na kutokana na kukosekana kwa alama hizo imekuwa vigumu kwa watumiaji barabara kujua maeneo hatarishi kwa kuwa hakuna alama zinazoonyesha tahadhari hizo.

Hata hivyo Luhanga alidai pia kwamba serikali imekuwa ikitumia kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya kugharamia matengenezo ya alama za barabarani na alama hizo hutumika kwa raia wote,hivyo kuziondoa ni kuwanyima haki raia wengine.

Katika maombolezi yake mshitakiwa kabla ya kusomewa adhabu hiyo,mshitakiwa alisema yeye binafsi hajaiba bomba hizo bali aliuziwa na mtu bila kujua kama bomba hizo ni mali ya serikali kwa ajili ya matumizi ya barabarani,hoja ambayo ilipingwa na Hakimu huyo kwamba haina mashiko kwa wakati huo.

Hata hivyo Haruna alisema kuwa kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa presha ya kushuka hivyo aliiomba Mahakama impunguzie adhabu na vile vile hilo ni kosa lake la kwanza hivyo Mahakama imfikiria na kumpunguzia na kumfikiria kumpa adhabu ndogo kutokana na matatizo hayo yanayomkabili.

Kabla yaa kutoa hukumu ya adhabu hiyo,Hakimu   Mkazi Mfawidhi,Ferdinand Kiwonde aliweka bayana kwamba baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili ameridhishwa kuwa mshitakiwa ni mkosaji  wa mara ya kwanza,ana presha ya kushuka lakini hakuwa na kielelezo chochote cha ushahidi wa kuthibitisha ugonjwa huo.

Hivyo Hakimu Kiwonde alisisitiza kwamba kisheria adhabu ya kosa hilo ni kifungo cha miaka mitatu jela,lakini kwa sababu hakuna kumbukumbu zozote za nyuma zinazoonyesha kuwa mshitakiwa huyo ni mkosaji mzoefu,hivyo Mahakama hiyo inampunguzia adhabu yake.

Akitoa hukumu,Hakimu wa Mahakama hiyo Kiwonde alimuhukumu Haruna Musa kuanza kutumikia adhabu ya mwaka mmojaa jela kwa kosa la wizi huo wa bomba tatu za alama za barabarani na kwamba yeyote Yule ambaye hatakuwa ameridhishwa na hukumu hiyo ana haki ya kukata rufaa.

No comments:

Post a Comment