Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, akizungumza na
wakazi wa kijiji cha Kisorya, wilaya ya Bunda alipokutana nao baada ya kukagua
ujenzi wa barabara ya Bulamba-Kisorya yenye urefu wa KM 51 inayojengwa kwa
kiwango cha lami, wilayani humo, mkoani Mara.
Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amemtaka mkandarasi
Nyanza Road Works kukamilisha ujenzi wa barabara ya Bulamba-Kisorya yenye urefu
wa KM 51 kwa kiwango cha lami ifikapo mwezi Novemba mwaka huu.
Prof.
Mbarawa ametoa kauli hiyo wakati akikagua ujenzi wa barabara hiyo na kuzungumza
na wananchi wa kijiji cha Kisorya na kusema kuwa usanifu wa barabara na
madaraja katika barabara hiyo umewasilishwa sasa ni jukumu la mkandarasi
kuendelea na ujenzi kwa kasi na kwa viwango vya ubora.
“Serikali
ina nia njema kwa wananchi wa wilaya ya Bunda na mkoa wa Mara sasa tunaijenga
barabara hii na mwishon mwa mwaka mtaanza kunufaika nayo”, amesema Waziri Prof.
Mbarawa.
Ameongeza
kuwa kukamilika kwa barabara hiyo utarahisisha mawasiliano na kupunguza gharama
za shughuli za usafirishaji wa samaki, mazao na abiria, uboreshaji makazi na
kukuza uchumi kwa maeneo yaliyo kando ya barabara.
Kuhusu
suala la fidia, Prof. Mbarawa amefafanua kuwa Serikali italipa fidia kwa
mwananchi ambaye barabara imemfuata kama anavyostahili.
“Serikali
haina nia ya kumuonea mtu yeyote bali inachofanya inalipa kulingana na sheria
inavyoelekeza”, amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.
Katika
hatua nyingine Waziri Prof. Mbarawa amekagua ujenzi wa barabara ya Makutano-Sanzale
KM 50 na kumwagiza mkandarasi wa M/S Mbutu JV Contractor (T) kuhakikisha
wanakamilisha mradi huo kabla ya mwezi Julai mwaka huu.
“Mradi
huu ni wa muda mrefu sana na wananchi wameusubiri kwa muda kama hamtamaliza
mradi huu mpaka mwezi juni, hii itakuwa kazi yenu ya mwisho, maana ninategemea
nyinyi kama wazawa mngekuwa wa mfano” amesisitiza Prof. Mbarawa.
Kwa
upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima amesema kwa sasa mkoa umeamua
kupata taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa miradi ya barabara kila baada ya miezi
mitatu ili kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati.
Naye
Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Mara, Mhandisi Mlima Ngaile
amesema Wakala utasimamia mradi wa ujenzi wa barabara hizo na kuhakikisha mradi
unazingatia viwango kulingana na mkataba.
Waziri
Prof. Mbarawa yuko mkoani Mara kwa ziara ya siku mbili akiwa na lengo la
kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya sekta ya Ujenzi,Uchukuzi na
Mawasiliano.
No comments:
Post a Comment