Samatta aumia tena na kutolewa dakika ya 36 tu genk ikishinda 3-1 ubelgiji - Mazingira FM

Mazingira Fm Live

Breaking News

Saturday, 10 February 2018

Samatta aumia tena na kutolewa dakika ya 36 tu genk ikishinda 3-1 ubelgiji


NAHODHA wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta jana amecheza kwa dakika 36 tu kabla ya kuumia na kutolewa, klabu yake, KRC Genk ikiibuka na ushindi wa 3-1 dhidi ya Zulte-Waregem kwenye mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji Uwanja wa Luminus Arena mjini Genk.
Samatta alitolewa dakika ya 36 na nafasi yake ikachukuliwa na mshambuliaji Mkongo, Dieumerci N'Dongala wakati huo timu hizo zikiwa zimefungana 1-1, Genk wakitangulia kwa bao la mshambuliaji Mgiriki, Nikolaos Karelis dakika ya 20 kabla ya mshambuliaji Mtunisia, Hamdi Harbaoui kuisawazishia Zulte-Waregem kwa penalti dakika ya 22.

Baada ya hapo, Genk ikafanikiwa kupata mabao mawili zaidi, yaliyofungwa na kiungo mkongwe wa umri wa miaka 36, Mbelgiji Thomas Buffel dakika ya 59 na kiungo Mspaniola, Alejandro Pozuelo Melero Pozuelo dakika ya 90 na ushei.
Samatta jana alikuwa anacheza kwa mara ya tano tu tangu apone maumivu ya mishipa midogo ya goti lake la mguu wa kulia iliyochanika Novemba 4, mwaka jana akiichezea KRC Genk ikilazimishwa sare ya 0-0 na Lokeren katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji Uwanja wa Luminus Arena mjini Genk na kumsababisha afanyiwe upasuaji mdogo. 
Kwa ujumla Samatta amefikisha mechi 75 tangu alipojiunga na Genk Januari mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Na katika mechi hizo, Samatta, mshambuliaji wa zamani wa Mbagala Market, African Lyon na Simba za Tanzania, amefunga mabao 22 kwenye mashindano yote.
Kikosi cha KRC Genk jana kilikuwa; Vukovic, Nastic, Colley, Aidoo, Maehle/Uronen dk78, Wouters, Seck, Pozuelo, Samatta/Ndongala dk36, Buffalo na Karelis/Malinovskyi dk83.
Zulte-Waregem: Bossut, Marcq/De Mets dk65, Derijck, Harbaoui, Kaya, Walsh/Leya Iseka dk86, Bjordal, Hamalainen, Koopman, Bongonda/Doumbia dk63 na Olayinka.

No comments:

Post a Comment