Familia
ya marehemu Akwilina Akwiline inaendelea na maandalizi ya mazishi,
huku ikielezwa kuwa Serikali imekubali kuyagharimia lakini si kutoa
fedha.
Serikali imefikia hatua hiyo baada ya jana Februari 20,2018 familia ya Akwilina kueleza kuwa bajeti ya mazishi ni Sh80 milioni.
Katibu
wa kamati ya mazishi Moi Kiyeyeu, ambaye ni kaka wa Akwilina amesema
Serikali imewajibu kuwa haitawapa fedha taslim bali itagharimia vitu
vilioorodheshwa katika bajeti ya mazishi hayo.
"Tulipotoa
bajeti hatukuwa na maana kuishinikiza Serikali itoe fedha zote bali
ilikuwa mahitaji ya msiba hadi pale utakapoisha. Tunashukuru Mungu kwa
Serikali kuridhia kugharimia," amesema Kiyeyeu.
Kuhusu
hilo, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia katika taarifa iliyotolewa
leo Februari 21,2018 imesema kupitia kwa Katibu Mkuu wake, Dk Leonard
Akwilapo ilipokea makisio ya gharama za mazishi ya Sh80 milioni kutoka
kwa msemaji wa familia, Festo Kavishe.
Mkuu
wa kitengo cha mawasiliano cha wizara hiyo, Mwasu Sware alisema baada
ya kupokea makisio hayo Dk Akwilapo alitahadharisha kuwa kuna baadhi ya
matumizi hayatakubaliwa kwa kuwa kisheria hayagharamiwi na Serikali.
Pia, katika makisio hayo kuna gharama ambazo zilikuwa zimepewa makadirio ya juu.
Alisema
katibu mkuu aliagiza kuwe na kikao kati ya wizara na ndugu wa marehemu
ili kuweka sawa changamoto hizo na kuwa na bajeti ya pamoja ambacho
kilifanyika jana jioni Februari 20,2018 na kufikia muafaka.
“Wizara inapenda kuufahamisha umma kuwa taratibu nyingine za maandalizi ya mazishi zinaendelea vizuri,” amesema.
Wakati
huohuo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison
Mwakyembe amefika nyumbani kwa dada wa marehemu Mbezi Luis kuhani msiba.
No comments:
Post a Comment