Viongozi wa Mkoa watakiwa kusimamia kazi ya usajili kwa ufanisi - Mazingira FM

Mazingira Fm Live

Breaking News

Sunday, 11 February 2018

Viongozi wa Mkoa watakiwa kusimamia kazi ya usajili kwa ufanisi

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dk Mwigulu Nchemba amewaagiza viongozi wa mkoa wa Morogoro kusimamia kazi ya usajili na utambuzi wa watu kwa ajili ya kupewa vitambulisho vya Taifa.

Dk Nchemba alitoa agizo hilo jana baada ya kuzindua kazi ya usajili na utambuzi inayofanywa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida).

Aliwataka viongozi wakiwamo watendaji na wenyeviti wa Serikali za mitaa kuhakikisha hakuna mtu ambaye si raia wa Tanzania anapewa kitambulisho.

Pia, aliwahakikishia wananchi kuwa wizara imejipanga kuhakikisha ifikapo Desemba 2018 wananchi wote hapa wenye miaka 18 na kuendelea watakuwa wameshasajiliwa na kupata namba za utambulisho.

Akielezea dhamira ya Serikali kuhusu kazi hiyo, alisema ni kuhakikisha wananchi wanatumia vitambulisho vya Taifa kwa matumizi mbalimbali na kusisitiza kuwa vitambulisho hivyo vinatolewa bure.

Akisoma taarifa ya utendaji kazi wa mamalaka hiyo, Kaimu mkurugezi Mkuu wa Nida, Andrew Massawe alisema tayari mashine 200 zimesambazwa ili kukidhi mahitaji ya usajili na kuhakikisha ifikapo Aprili 30 mwaka huu kazi iwe imekamilika.

Pia, alisema Nida imetoa ajira za muda mfupi kwa wananchi 200 na kufungua ofisi kwenye wilaya zote.

Alisema jumla ya maofisa 23 wa kudumu kutoka Nida wamegawanywa kwenye wilaya zote kwa lengo la kusaidiana na watendaji wengine kuhakikisha kazi hiyo inafanikiwa.

Massawe alieleza baadhi ya faida za kuwa na kitambulisho cha Taifa kuwa ni pamoja na kuweza kupata huduma kirahisi za afya, elimu na fedha.

Kaimu mkurugenzi huyo aliitaja mikoa ambayo imefanya vizuri katika kazi hiyo ya usajili na utambuzi kuwa ni Iringa, Mara, Simiyu, Arusha, Geita, Mwanza, Ruvuma, Kilimanjaro pamoja na Lindi.

Alisema mafanikio hayo yalitokana na uongozi madhubuti wa mikoa hiyo.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Stephen Kebwe alisema jumla ya wakazi 961,309 wenye miaka 18 na kuendelea watasajiliwa.

Hata hivyo alisema katika kipindi hiki cha kilimo kunaweza kuwa na changamoto kwa wananchi kujitokeza kwani wengi watakuwa shamba.

No comments:

Post a Comment