WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Manispaa ya Dodoma imekamilisha upimaji wa viwanja vipya zaidi ya 15,000 na vitaanza kugawiwa Machi, 30 mwaka huu.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo jana (Ijumaa, Februari 9, 2018) bungeni mjini Dodoma wakati akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa 10 wa Bunge la 11. Bunge limeahirishwa hadi Aprili 3, mwaka huu.
“Kutokana na agizo la Serikali la kuhamishia makao makuu ya nchi Dodoma, mahitaji ya viwanja hadi Februari 2018 yalikuwa ni viwanja 24,602. Manispaa ya Dodoma hivi sasa inatekeleza mkakati wake wa kuzalisha viwanja 30,000 kwa kushirikiana na wadau mbalimbali. Tayari upimaji wa viwanja vipya 15,316 umekamilika na vitaanza kugawiwa kuanzia tarehe 30 Machi 2018,” amesema Waziri Mkuu.
Amelieleza Bunge kwamba kiasi kilichobaki cha viwanja 14,684 kitakamilika ifikapo Juni, 2018 na wananchi watauziwa viwanja hivyo kwa bei elekezi itakayotolewa na Manispaa hiyo.
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwasihi wananchi na watumishi wa umma watakaohitaji viwanja kufuata taratibu za maombi ya viwanja pindi vitakapotangazwa rasmi na kusisitiza kuwa zoezi la kubadilisha hati zilizotolewa na iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) na kupata hatimiliki za miaka 99 linaendelea. “Wenye hati za CDA mnasisitizwa kuendelea na taratibu za kuzibadilisha,” amesema.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema jumla ya watumishi 3,829 kutoka wizara na taasisi mbalimbali za Serikali tayari wamehamia Dodoma akiwemo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.
“Napenda kulifahamisha Bunge lako tukufu kuwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na ofisi yake walihamia rasmi Dodoma tarehe 15 Desemba, 2017 kama ilivyopangwa,” amesema.
Kuhusu mpango wa kuifanya Dodoma kuwa ya kijani, Waziri Mkuu amesema Serikali imedhamiria kuifanya Dodoma iwe na ukanda wa kijani (Green Belt) kupitia mpango wa kuendeleza, kutunza na kuhifadhi maeneo ya msitu wa Mahomanyika wenye ukubwa wa hekta 2,000; msitu wa Chimwaga Nzuguni (hekta 300) na msitu wa Mbwenzelo (hekta 3,500) pamoja na vilima vya Image na Nyankali.
“Katika kutimiza malengo hayo ya kuifanya Dodoma kuwa ya kijani, Serikali imeendelea kutoa elimu ya upandaji miti na uhifadhi wa misitu hususan miti adimu ya asili na makao ya wanyamapori mbalimbali katika kata nane za Ipala, Nzuguni, Kikombo, Ng’ong’ona, Chahwa, Zuzu, Hombolo na Kikuyu Kaskazini ambapo kila kata imepewa lengo la kupanda miti isiyopungua 40,000,” amesema.
Kuhusu zoezi la upandaji miti, Waziri Mkuu amesema miche 34,000 yenye thamani ya sh. milioni 34 ilitolewa bure katika kata mbalimbali na kupitia mradi wa TASAF miche mingine 138,000 inaendelea kusambazwa kwa wananchi. “Kwa sasa, Manispaa ya Dodoma inaendelea na maandalizi ya kuotesha miche mingine 200,000 kwa ajili ya msimu ujao,” ameongeza.
Ametumia fursa hiyo kuwashukuru Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Bonde la Wami Ruvu, Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) ambao kwa kushirikiana na Manispaa ya Dodoma wamefanikisha upandaji wa miche 79,000 katika maeneo ya UDOM, Mzakwe, Iseni Park, Nala na Mahomanyika.
Katika kuhakikisha zoezi la upandaji miti linakuwa endelevu, Waziri Mkuu ameziagiza Halmashauri zote nchini zihakikishe zinaandaa miche ya kutosha na kuweka utaratibu wa kila kaya kupanda na kutunza miti isiyopungua mitano.
“Taarifa za utendaji na maendeleo za Halmashauri zote zioneshe mafanikio yaliyopatikana kutokana na zoezi la upandaji miti. Utendaji wa Wakurugenzi na Wakuu wote wa Mikoa na Wilaya, utapimwa kutokana na uendelezaji na utunzaji wa mazingira katika maeneo yao,” amesisitiza.
No comments:
Post a Comment