WANANCHI wa wilaya ya Kwimba
wamemuomba Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aondoke na mkuu wa wilaya hiyo Bw. Mtemi
Msafiri baada ya kutoridhishwa na utendaji wake.
Wametoa ombi hilo jana (Ijumaa,
Februari 16, 2018) walipozuia msafara wa Waziri Mkuu alipowasili katika Ofisi
za Halmashauri ya wilaya Kwimba zilizopo Ngudu kwa ajili ya kuzungumza na
watumishi akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza.
Wananchi hao walimkataa mkuu wao wa
wilaya Bw. Msafiri kupitia ujumbe wa mabango 17, ambapo Waziri Mkuu amewataka
wananchi hao wawe watulivu wakati Serikali inafanyia kazi malalamiko yao.
Wananchi hao wanadai kwamba Mkuu
huyo wa Wilaya anatabia ya kuamrisha polisi wawakamate kwa kisingizio cha
uzururaji na kisha wanawekwa mahabusu, ambapo baada ya muda wanatolewa na
kwenda kulima kwenye shamba lake.
Waziri Mkuu amesema Serikali
inahitaji kila mtumishi atambue majukumu yake na ayatekeleze. “Hakuna
atakayeonewa, haki zenu zote tunazitekeleza nanyi mnatakiwa kutenda haki kwa
kuwatumikia wananchi.”
Hata hivyo, Waziri Mkuu amewataka
Mkuu huyo wa wilaya Bw. Msafiri, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya
ya Kwimba Bibi Pendo Malebeja na wakuu wote wa Idara wajitathmini kama kweli
wanatekeleza majukumu yao ipasavyo na kuwatumikia wananchi.
“Mkurugenzi katika kipindi chako
chote cha utendaji kuanzia mwaka 2013 hadi leo, fedha nyingi za Serikali
zilizoletwa Kwimba zimepotea na hazijulikani zilipo huku miradi mingi bado haijakamilika
na muda wote huo Halmashauri imekuwa inapata hati chafu.”
Pia Waziri Mkuu amewataka watumishi
wote wa Halmashauri ya wilaya ya Kwimba wabadilishe mienendo yao na wawatumikie
vizuri wananchi pamoja na kuishi nao vizuri.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
IJUMAA, FEBRUARI 16, 2018.
No comments:
Post a Comment