Ameidawa kuwa serikali haitatoa shilingi milioni 50 kwa kila kijiji na mitaa-Bunda Mara - Mazingira FM

Mazingira Fm Live

Breaking News

Tuesday, 13 March 2018

Ameidawa kuwa serikali haitatoa shilingi milioni 50 kwa kila kijiji na mitaa-Bunda Mara



MBUNGE wa jimbo la Bunda vijijini , Bonfas Getere amedai serikali haitatoa shilingi milioni 50 kwa kila kijiji na mitaa na pensheni za wazee ambao si watumishi wa umma kwa kuwa fedha hizo zimeelekezwa katika miradi mingine.

Amesema fedha hizo, rais ameelekeza katika ujenzi wa vituo vya afya, uimarishaji wa reli ya kati na ujenzi wa barabara za juu kupunguza msongano jijini Dar Es Salaam.

“Labda niwaweke wazi kama mbunge wenu kuhusu ahadi ya rais ya kutoa shilingi milioni 50 kwa kila kijiji na pensheni za wazee……..fedha hizi hazitatolewa katika mfumo huo, badala yake zimeelekezwa katika kuimarisha miundombinu ya jamii” alisema Getere.

“Miongoni mwa fedha hizo alizoahidi rais wetu ndizo hizi shilingi milioni 400 za ujenzi wa kituo cha afya, zingine zimenunua vichwa vya treni, viko pale Dar Es Salaam na kujenga mradi wa ‘fly over’ kupunguza msongamano jijini Dar Es Salaam……. Naomba tuelewe hivyo”. Alisisitiza mbunge.

Getere amesema hayo hivi karibuni katika Kijiji cha Nyang’aranga kwenye ujenzi wa kituo cha afya, ambapo mzee Charles Kiraryo Maro(86) alimuuliza mkuu wa wilaya ya Bunda, Lydia Bupilipili kutaka kujua ni lini serikali itatekeleza ahadi yake ya kuwalipa pensheni wazee wasiojiweza.

Mzee Kimaro amedai anasikia baadhi ya wazee wanalipwa pensheni hizo katika maeneo mengine.

Hata hivyo licha Mbunge huyo kutoa majibu hayo, Mkuu wa wilaya amemwahidi Mzee Kimaro kumpa nafasi ili aende kujiridhisha katika ilani ya uchaguzi wa mwaka 2015 kuhusu utekelezaji wa ahadi hizo.

Badala yake DC huyo amemweleza Mzee Kimaro kuwa anachojua ni bima ya matibabu ya wazee na kwamba afuatilie kwa watendaji wa vijiji na kata ili wawasilishe jina lake kwa mganga mkuu wa wilaya kwa ajili ya kumpa kitambulisho ya kupata huduma hiyo bure.

No comments:

Post a Comment