Mbunge wa jimbo la Bunda mjini Ester Amos Bulaya amesema kwakuwa serikali wameshindwa kuweka fensi katika mpaka wa hifadhi ya wanyama Serengeti kuzuia Tembo kuingia katika makazi ya watu wanaopakana na hifadhi hiyo atafatilia kufahamu ukweli kuhusu zao la Pareto kuzuia wanyama hao kuingia katika makazi ya watu na kuvuruga mashamba yao.
Bulaya amesema hayo Jana ofisini kwake wakati akifanya mahojiano na mwandishi wa radio Mazingira fm ambapo amedai kuwa wakazi wa mji wa Bunda hawapendi kuombaomba misaada ya chakula lakini jitihada zao za kujituma katika kilimo zinakwamishwa na wanyama hao kuvamia mashamba na kuharibu mazao yao.
Amesema mbali na hasara kubwa wanayopata wakulima hao lakini bado serikali haiwatendei haki kwa malipo wanayopewa na mbaya zaidi ni kucheleweshwa kwa malipo hayo.
Amesema msaada anaoufikiria kwa sasa kuwasaidia wananchi wake wanaokabiliwa na changamoto hiyo hasa Kata ya Kunzugu, Nyatwari, na Balili ni kufuatilia kwa karibu kubaini Kama zao hilo la Pareto linafukuza tembo, watafanya mpango wa kupanda katika mpaka ili kuwazauia tembo kuingia katika mashamba na makazi ya wananchi.
Hata hivyo tembo kwa msimu huu ambao wakulima wengi wamelima zao la pamba wameelezwa kuwa mara nyingi wamekuwa wakivamia mashamba ya wakulima na hivyo kupelekea wananchi hao kuhofia kushindwa kulipa madeni ya mikopo ya pembejeo walizochukua kupitia kilimo cha mkataba baina yao na makampuni ya zao hilo la pamba.
No comments:
Post a Comment