MSICHANA mwenye umri wa miaka 14,
amejisalimisha mwenyewe katika Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Nkasi mkoani
Rukwa akipinga uamuzi wa wazazi wake wa kumuozesha kwa nguvu kwa mzee mwenye
umri wa miaka 75, Mtokambali Chele, badala yake anataka apelekwe shule aanze
kusoma.
Taarifa za uhakika kutoka eneo la
tukio, zinaeleza kuwa baba mzazi wa msichana huyo, Matembezi Mugo, inadaiwa
awali alimuozesha dada ya msichana huyo mwenye umri wa miaka 16 kwa Mzee Chele,
lakini alifanikiwa kutoroka kwa mumewe huyo baada ya kubaini kuwa kumbe ni mzee
sana.
Aidha, msichana huyo alibaini kuwa
mume wake huyo alikuwa na wake wengine wanne waliomzalia watoto ambao idadi yao
inakadiriwa kuwa zaidi ya 50.
Akizungumza na gazeti la Habarileo,
Kamanda wa Polisi wa Mkoa, George Kyando alithibitisha kutokea kwa mkasa huo,
na kufafanua kuwa msichana huyo alijisalimisha kituoni hapo wiki iliyopita
akipinga uamuzi wa wazazi wake kumuozesha kwa nguvu kwa mzee huyo ambaye ni mkazi
wa Kijiji cha Swaila wilayani Nkasi.
Akisimulia alisema mzazi wa
kiume wa msichana huyo, mwishoni mwa mwaka jana alimuozesha binti yake mwenye
umri wa miaka 16 kwa Mzee Chele ambaye tayari alikuwa na wake wanne na watoto
wanaokadiriwa kufikia 50 na idadi isiyojulikana ya wajukuu na vitukuu.
Majirani wa Mugo ambao kwa masharti
ya kutoandikwa majina yao gazetini, walilieleza gazeti hili kwa nyakati tofauti
kuwa kuwa alimuozesha binti yake huyo mwenye umri wa miaka 16 kwa mahari ya
ng’ombe 50.
Wanadai kuwa mke wa kwanza wa Mzee
Chele ana watoto 14, wa pili ana watoto 13, watatu ana watoto 12 na wanne ana
watoto 11.
“Msichana huyo mwenye umri wa miaka
16 ambaye ni dada yake na huyo msichana mwenye umri wa miaka 14 alipofikishwa
nyumbani kwa “mumewe” (Chele) alibaini kuwa ni mzee sana isitoshe tayari
alikuwa na wake wanne na watoto wengi tu ...akaamua kutoroka na kukimbilia
kusikojulikana,” alieleza Kamanda Kyando.
Aliongeza kuwa baada ya msichana
huyo kutoroka nyumbani kwa ‘mumewe’ huyo kijijini Swaila, Mzee Chele alimwendea
baba mzazi wa msichana huyo na kumtaka amrejeshe mahari yake yote kwa kuwa
binti yake ametoroka nyumbani kwake.
“Ndipo Mzee Mugo alipomtuliza
mzee mwenzake Chele kuwa atampatia binti mwingine ambaye ndiyo huyu mwenyewe
miaka 14 akazibe pengo la dada yake aliloliacha nyumbani kwa Mzee Chele baada
ya kutoroka... hakuwa tayari kurejesha mahari,” alieleza Kamanda Kyando.
Aliongeza kuwa kwa usalama wa
binti huyo aliyejisalimisha katika Kituo cha Polisi ambako sasa anahifadhiwa kwa
muda na Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto la Wilaya ya Nkasi, Anna Kisimba
nyumbani kwake. Kutokana na mkasa huo, Kamanda Kyando alithibitisha kuwa tayari
Mzee Chele ameshakamatwa.
No comments:
Post a Comment