Mkazi mmoja wa kijiji na kata ya
Kinaga, Kahama mkoani Shinyanga amechunwa ngozi ya sehemu za siri baada ya
kuleweshwa kwa pombe.
Watu waliomchuna mkazi huyo
anayejulikana kwa jina la Paschal Misana, wametoweka na hadi sasa
hawajajulikana.
Diwani wa kata hiyo, Mary Manyambo
alisema tukio hilo lilitokea Aprili 16, baada ya Misana kupigiwa simu na mtu
aliyekuwa akimdai Sh200,000.
“Lakini kwa maelezo ya muathirika ni
kuwa baada ya kufika nyumbani kwa mtu huyo alinyweshwa pombe hadi akapoteza
fahamu na alizinduka asubuhi ya siku iliyofuata, akajikuta amechunwa uume wake
kuanzia kwenye korodani,” alisema Manyambo.
Mganga wa zamu katika Hospitali ya
Mji wa Kahama, Dk Abdallah Simba alisema jana kuwa mtu huyo alifikishwa hapo
juzi mchana akiwa na hali mbaya.
“Aliletwa hapa sehemu yake ya uume
ilikuwa imekatwa kwa kuzunguka na kisha kunyofolewa ngozi yote ya sehemu hizo
hali iliyosababisha kuvuja damu nyingi,” alisema.
“Wachunaji hao walimkata kitaalamu
kwani hawakufika kwenye mishipa ya sehemu za siri na hivyo tayari ameshonwa na
kurudishiwa alipokuwa amekatwa wakati wa kuchunwa.
“Sehemu zake za siri zinaweza
kuendelea kufanya kazi kama kawaida kwa sababu sehemu za mishipa hazikukatwa.”
Akizungumzia tukio hilo akiwa
hospitalini hapo anapoendelea na matibabu, Misana alisema baada ya kupigiwa
simu hiyo alikwenda kwa lengo la kulipwa fedha alizokuwa amemkopesha mtu huyo.
“Nilimkopesha ng’ombe mmoja kwa
thamani ya Sh200,000 na nilipofika baiskeli yangu iliingizwa chumbani na kisha nikakaribishwa
ndani,” alisema.
Misana alisema baada ya kukaa,
aliwaona wageni watatu waliokuwa chumbani, wawili wakiwa wanawake.
Alisema baadaye alitengewa ugali
ambao alikula na wenyeji na baada ya kumaliza alipewa pombe aina ya shujaa
waliyokuwa wakipewa pia wageni wengine.
Majeruhi huyo alisema baada ya
kunywa pombe hiyo alipoteza fahamu mpaka asubuhi alipozinduliwa na mke wa
mtuhumiwa.
Hata hivyo, alisema alishangazwa na
kitendo cha kuwa peke yake akiwa uchi, huku akitokwa damu na sehemu zake za
siri zikiuma.
“Sikujua chochote, baada ya watu
kujaa wasamaria wema na kuanza kunipa huduma ya kwanza, walinieleza kuwa sehemu
zangu za siri zilikuwa zimekatwa, hali iliyonishtua na baadaye polisi walifika
wakanichukua na kunipeleka hospitalini,” alisema.
Kamanda wa polisi wa mkoa, Simon
Haule alisema tayari wanamshikilia mtuhumiwa kwa ajili ya mahojiano.
Baada ya kuhojiwa, mtuhumiwa huyo
alisema wageni wake watatu walihusika kumchuna ngozi Misana na kutoweka nayo na
mpaka alipokamatwa hajui walielekea wapi.
Polisi wanaendelea kuwasaka wageni
hao huku mtuhumiwa akiendelea kusaidia upelelezi.
No comments:
Post a Comment