Askofu wa Kanisa la Kiinjili la
Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Njombe, Isaya Mengele, amesema kuwa
kitendo kilichofanywa na baadhi ya waumini wa kanisa hilo Dayosisi ya Ziwa Tanganyika
kumjeruhi kwa kumpiga mawe Askofu wa KKKT Dayosisi ya Tanganyika, Ambele
Mwaipopo,limelitia doa kanisa hilo na kinapaswa kulaaniwa.
Akizungumza jana katika ibada maalum
iliyofanyika katika Kanisa la Kiaskofu la KKKT Usharika wa Sumbawanga Mjini,
Askofu Mengele ambaye ni Mwenyekiti wa maaskofu wa KKKT Kanda ya Kusini,
alisema ni aibu kubwa na fedheha kwa dayosisi hiyo yenye miaka minne tangu
kuanzishwa kwake na waumini hao wanapaswa kutubu na kuomba radhi.
Alisema kuwa pia yeye ataongoza
ujumbe wa maaskofu wa kanda hiyo kwenda kwa Rais John Magufuli kumuomba radhi
kwa kitendo cha baadhi ya waumini hao kuvuruga amani ambayo serikali yake
imekuwa ikiihimiza kwa kitendo cha kumjeruhi kwa kumpiga mawe Askofu Mwaipopo.
Pia Askofu alimshauri Askofu
Mwaipopo kuvunja Baraza la Dayosisi hiyo kwa kuwa baadhi ya wajumbe wake
wamekuwa ni chanzo cha mgogoro uliopo katika kanisa hilo na wamekosa utii
kwake.
Muda mfupi kabla maaskofu sita
wanaounda Kanda ya Kusini ya KKKT hawajafika kuongoza ibada ya jana na kumpa
pole Askofu Mwaipopo kwa kujeruhiwa, baadhi ya waumini waliingia katika kanisa
hilo na kuondoa kiti maalum cha kukalia askofu huyo wakati wa kuongoza ibada.
Maaskofu hao ni Renald Mtenji wa
Ulanga Kilombero, Askofu Blastone Gaville (Dayosisi ya Dira-Iringa), Askofu Job
Mbwilo (Dayosisi ya Kusini Magharibi- Matamba), Askofu Amon Mwenda (Dayosisi ya
Ruvuma), Askofu Edward Mwaikali (Dayosisi ya Konde Mbeya) na Askofu Isaya
Mengele (Dayosisi ya Kusini Njombe).
Lengo la jopo hilo la maaskofu hao
limefika kumpa pole Askofu Mwaipopo na kuwasihi waumini waache mara moja
vitendo vya uvunjifu wa amani kwa kuwa vinaliumiza na kulichafua kanisa hilo
ambalo lina zaidi ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwake nchini.
Katika ibada hiyo Katibu wa Dayosisi
ya Ziwa Tanganyika, Fredrick Lazaro, alisoma tamko maalum la Halmashauri Kuu
kwa wakristo wa Usharika wa Kathedral Sumbawanga Mjini kuekeleza waumini 21 na
watumishi wa kanisa hilo kuwa wamejitenga na kanisa hilo kwa muda usiojulikana.
Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa,
Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Dk. Alfan Haule, alisema vitendo vya uvunjifu wa
amani havitafumbiwa macho na serikali na kama vitaendelea, itatumia vyombo
vyake vya ulinzi na usalama kuvidhibiti.
Dk. Khaule aliagiza kuwa wote
walioiba kiti cha Askofu Mwaipopo wasakwe na wakamatwe, ili wafikishwe mbele ya
sheria wachukuliwe hatua kwani kitendo cha kuiba kiti hicho ni wizi kama wizi
mwingine wowote.
Mei 7, mwaka huu, Askofu Mwaipopo
alifukuzwa kwa mawe baada ya baadhi ya waumini kumzuia kuingia usharikani
wakidai hawataki kumuona akiwepo eneo la kanisa la Usharika wa Simbawanga
Mjini.
No comments:
Post a Comment