Mbunge
Bunda Mjini (Chadema), Ester Bulaya amesema Serikali ya Awamu ya Tano
tangu ilipoingia madarakani Novemba 5, 2015 imelifanya Shirika la Umeme
Tanzania (Tanesco) kushindwa kujiendesha kwa faida, kutaka ligawanywe.
Bulaya
ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Mei 24, 2018 bungeni mjini Dodoma katika
mjadala wa bajeti ya Wizara ya Nishati mwaka 2018/19.
Amesema
kwa muda mrefu ripoti mbalimbali za kamati za Bunge, ikiwamo ya
mashirika ya umma, zinaeleza namna Tanesco inavyojiendesha kwa hasara.
Amesema
kabla ya Serikali hiyo haijaingia madarakani, Tanesco ilikuwa ikipata
hasara ya Sh124 bilioni lakini baada ya kuingia madarakani Tanesco
inapata hasara ya Sh346 bilioni inayotokana na upugufu wa maji na
gharama za uendeshaji.
“Tanesco
ina madeni ambayo yamepanda kwa asilimia 23. Kabla Serikali hii
haijaingia madarakani, Tanesco walikuwa na madeni ya Sh738 bilioni
lakini baada ya kuingia yamefikia Sh958 bilioni na haya si maneno ya
Bulaya. Ukiangalia ripoti ya CAG, inasema madeni hayana uhusiano kati ya
Tanesco na mali, kwa maana nyingine Tanesco imefirisika,” amesema
Bulaya.
Amesema
wakati madeni haya yanatokea, kulikuwa na ushauri na mikakati
mbalimbali ya kuligawanya shirika hilo ili kutenganisha usambazaji na
uzalishaji.
“Leo
hii tusingekuwa tunazungumza umeme wa vibaba wakati tunataka Tanzania
ya viwanda. Wakati haya yanafanyika, Tanesco inashindwa kukusanya madeni
makubwa, Tanesco inaidai Hospitali ya Tumaini Dola milioni 9.4 za
marekani sawa na Sh18 bilioni na ni kodi ya pango,” amesema.
“Kodi
hii ni tangu mwaka 1998 haijawahi kulipwa, kulikuwa na kesi mahakamani
na Tanesco ikashinda na mahakama imeitaka kuondoka lakini mpaka sasa
haijachukua hatua zozote.”
Mbunge
huyo pia alihoji kitengo cha wizara hiyo kutenga Sh700 bilioni kwa
ajili ya mradi wa umeme wa Stiegler’s Gorge badala ya fedha hizo
kuzipeleka Rea (Wakala wa Umeme Vijijini) na Tanesco.
No comments:
Post a Comment