WAKULIMA wa zao la pamba wilayani Bunda mkoani Mara hadi sasa wamegoma kuuza pamba zao kwa vyama vya msingi kwa kile wanachodai kuwa hawana imani na vyama hivyo ambavyo viliwadhuluma hapo awali.
Kitendo hicho kimewafanya baadhi ya mawakala wa makampuni waliojitayarisha katika vituo mbalimbali kushirikiana na vyama vya msingi kufunga virago vyao baada ya kukaa vituoni bila kuwaona wauzaji.
Hali hii imetokea katika vijiji vya Kunzugu, Bukole, Miale,Nyamatoke na baadhi ya maeneo huku wakiishutumu vikali serikali kuwa imechukua hatua za haraka kukabidhi majukumu hayo kwa vyama vya msingi kabla ya kufanya utafiti wa kina.
Aidha wakulima hao wamedai hawatauza pamba zao huku baadhi yao wakisema kuwa hali hiyo ikiendelea watahaahirisha kulima zao hilo katika msimu ujao na kwamba serikali inachangia kuandaa kifo cha zao hilo maarufu ya biashara.
Shija Maduhu(48) mkazi wa Kijiji cha Bukole akizungumza na mwandishi wa habari hizi alidai wakulima hawako tayari kuuza zao hilo kwa mfumo wa sasa hadi serikali ione umuhimu wa kufanya marekebisho.
“Tumetishwa na hali hii, kwanza vyama hivi vya msingi vya wakulima vilitunyanyasa sana katika kipindi kilichopita, fedha zetu zililiwa kwa mfumo huu………” alisema Maduhu.
“ we ni mwandishi wa habari, unajua wazi kwamba kutokana na mfumo huu wa kuuza zao lako na fedha kuchukuliwa baadaye wakulima walidhulumiwa mpaka mali ya vyama hivi vilitaifishwa kutokana na madeni, leo bila kupitia mchakato imara mfumo ule unarudishwa, kwa kweli serikali itusamehe katika hili.
“Mara Co-operative Union (MCU) kiko wapi, nani alikiua, tuna jineri hapa ya Ushashi bado iko chini ya mfilisi vyote vilivyouawa na mfumo huu wa vyama vya msingi…. Ni vyema serikali ingekaa nasi tujadiliane tufanye nini” alisisitiza.
Aidha alidai kitendo cha agizo la serikali la kutaka kila mkulima wa pamba afungue akaunti ili fedha za mauzo yake yatumwe kwenye akaunti yake inalenga fedha hizo kukatwa bila ridhaa za wakulima.
Wamedai walilima kwa furaha wakitegemea kupata fedha lakini matumaini yao yanaendelea kufifia huku wakikabiliwa na hali ngumu ya uchumi wakati ambapo wanafanya matayarisha ya kuwapeleka shule watoto katika muhula wa pili unaoanza mwezi Julai.
Hivi karibuni akifungua msimu wa mauzo ya pamba mkoani Mara katika Kijiji cha Bukole wilayani Bunda , mkuu wa mkoa wa Mara aliagiza kila mkulima wa pamba kuhakikisha anafungua akaunti benki ili atakapouza pamba yake fedha zake ziwekwe kwenye akaunti yake na si vinginevyo.
Pia Malima alitoa tahadhari kuwa mkulima yeyote ambaye atauza pamba zake holela au kwa kampuni yoyote bila kupitia vyama vya msingi atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Mkuu wa wilaya ya Bunda, Lydia Bupilipili na watendaji wake wilayani Bunda inawasisitizia wakulima wa Bunda kuuza pamba zao katika vyama vya ushirika ingawa toka msimu wa manunuzi ufunguliwe Mei Mosi mwaka huu bado wakulima wengi hawajauza pamba zao.
No comments:
Post a Comment