Wakulima wa Pamba Kunzugu wamekubali yaishe!!!! - Mazingira FM

Mazingira Fm Live

Breaking News

Tuesday, 27 June 2023

Wakulima wa Pamba Kunzugu wamekubali yaishe!!!!

Wakulima wa zao la Pamba kata ya Kunzugu Halmashauri ya mji wa Bunda mkoani Mara wamesema kutokana na ugumu wa maisha wameshindwa kuendelea kusubiri bei ya pamba ipande na badala yake wameamua kuuza kwa bei elekezi ya shilingi 1060

Wakizungumza na Radio Mazingira Fm jumapili hii 25 June 2023 katika ofisi za AMCOS Kunzugu 'Kituo B' wakati wakiuza pamba wakulima hao wamesema wamesubiri kwa muda mrefu kuona ushindani wa makampuni katika kupandisha bei lakini mpaka sasa hakuna kampuni iliyojitokeza kulipa zaidi ya bei elekezi ya shilingi 1060 iliyotangazwa na serikali.

Pambano Henga ni mkulima wa Pamba kata ya Kunzugu

"Kwa bei ya shilingi 1060 naona kwangu ni kama mzigo kwasababu ninapouza kilo 10 haikidhi mahitaji yangu kwahiyo pamba nimeshauza kulingana na shida niliyonayo hususani njaa" alisema Pambano Henga ambaye ni mkulima wa pamba.

Chaba Charles Chaba ni mkulima wa Pamba amesema "kulingana na matarajio yangu mwaka huu nilitarajia bei itakuwa kama mwaka jana lakini nimejikuta nanawia kalai, kwasababu mwaka jana tulikuwa na bei ya shilingi 2000 kwa kilo lakini mwaka huu imeshuka hadi kufikia shilingi 1060 kwa kilo kwahiyo nimeshindwa kufanya nilichotarajia baada ya kuuza pamba".

Wakulima wakiwa katika ofisi za AMCOS Kunzugu kwa ajili ya kuuza pamba

Mazingira Fm imezungumza na Katibu wa AMCOS katika kituo hicho, Nyang'era Lukiko amesema zoezi la ununuzi wa pamba wameanza tarehe 26 May 2023  ambapo wakulima walianza kwa kusuasua wakilalamikia bei iliyotangazwa lakini mpaka sasa wamenunua zaidi ya kilo 136,000 kutokana na ugumu wa maisha wengi wao wameshindwa kusubiri na kulazimika kuuza kwa bei iliyopo hivyo pamba katika eneo lao inakaribia kuisha.

Nyang'era amesema walitegemea kampuni 9 za ununuzi wa pamba wilaya ya Bunda zitashindana katika kupandisha bei ya pamba lakini mpaka sasa hazina ushindani badala yake kila kampuni inapanga foleni kwa AMCOS kwamba ikitoka kampuni fulani nyingine ikusanyiwe kwa bei hiyo hiyo ya shilingi 1060.


No comments:

Post a Comment