“Serikali itusaidie kampuni ya ujenzi ya China iturekebishie nyumba zetu zilizoharibika wakati wakilipua miamba kutengenezea barabara ya Nyamuswa” wakazi wa Misisi wilaya ya Bunda
Na Edward Lucas
Wakazi wa mtaa wa Misisi kata ya Sazira Halmashauri ya Mji wa Bunda mkoani Mara wameiomba serikali ielekeze na kuisimamia kampuni ya ujenzi ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC), iliyokuwa inajenga barabara ya kipande cha Bulamba Nyamuswa iwafanyie maboresho ya nyumba zao zilizoharibika kutoka na shughuli ya ulipuaji wa miamba ili kupata kokoto za ujenzi wa barabara kutoka katika eneo hilo.
wakazi hao ambao wanaishi karibu na ziliposimikwa mashine za kuchakata kokoto (karasha)wamesema wamejikuta katika mazingira magumu baada ya nyumba zao kubaki na nyufa, mabati kuharibika pamoja na adha zingine jambo linalowasababishia hofu kubwa ya kuendelea kuishi kwenye nyumba hizo
Mwenyekiti wa mtaa wa Misisi, Amos Mashamba Mgongo amekiri kuwepo kwa malalamiko hayo kutoka katika kaya zipatazo 20 na kueleza kuwa baadhi ya wananchi katika kaya zipatazo 4 walilipwa fidia ili kupisha kwa muda huku wengine wakiahidiwa kufanyiwa marekebisho kutokana na uharibifu utakaokuwa umejitokeza baada ya kumaliza shughuli za ujenzi lakini mpaka sasa hakuna dalili ya kufanyika marekebisho hayo.
Kwa upande wake Diwani wa kata hiyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Bunda, Mhe. Michael Kweka amesema ni kweli kulikuwepo na malalamiko ya wananchi kupata adha ya vumbi, nyumba kuharibika na changamoto zingine za kiafya ambapo baada ya tathmini baadhi walilipwa ili kupisha kwa muda katika eneo hilo huku akiahidi kufuatilia malalamiko ya wananchi na kuyawasilisha katika mamlaka husika.
No comments:
Post a Comment