Kampeni ya chakula shuleni yapelekea shule 11 bunda tc kufuta daraja 0
27 February 2025,

Yapo mabadiliko makubwa ya kitaaluma tangu sera ya wanafunzi kupata chakula shuleni ambapo kati shule 17 za sekondari za halmashauri ya mji wa Bunda shule 11 zimefanikiwa kufuta daraja sifuri kwa matokeo kidato cha nne.
Na Adelinus Banenwa
Mbunge wa jimbo la Bunda mjini Mhe Robert Chacha Maboto amewataka wazazi wa wanafunzi katika jimbo la Bunda mjini kufanya kila linalowezekana kuhakikisha wanachanga chakula cha wanafunzi shuleni kama wanahitaji matokeo mazuri kwa watoto wao.
Kauli hiyo ameitoa leo tarehe 26 Feb 2025 katika siku ya tatu ya ziara yake iliyokuwa inalenga kuhamasisha chakula shuleni huku katika siku hizo tatu Mhe mbunge ametembelea jumla ya shule za sekondari 16.

Mhe Maboto amesema hakuna ambaye hafahamu juu ya ugumu wa maisha lakini suala la chakula shuleni ni jambo la mzazi kuelewa na kuamua endapo anataka matokeo mazuri ya mtoto hasa kitaaluma hivyo kila mzazi anao wajibu wa kitimiza majukumu yake.
Afisa lishe halmashauri ya mji wa Bunda Bi Lucy Erasto Mwalwayo amesema yapo madhara mbalimbali ya muda mrefu ambayo yatampata mtoto endapo atakaa muda mrefu bila kupata chakula shuleni ambapo amesema madhara hayo ni pamoja na kuwa na tabia ya kuishiwa damu pindi atakapofikia kipindi cha kuzaa kwa watoto wa kike, upungufu wa nguvu za kiume kwa watoto wa kiume, vidonda sugu vya tumbo pamoja na kupata saratani ya utumbo.

Kwa upande wake Sauda Mwakyembe kaimu afisa elimu sekondari kwa upande wa halmashauri ya mji wa Bunda amesema yapo mabadiliko makubwa ya kitaaluma tangu sera ya wanafunzi kupata chakula shuleni ambapo kwa matokeo ya kidato cha nne mwaka 2024 kwa shule zote 17 za sekondari za halmashauri ya mji wa Bunda shule 11 zimefanikiwa kufuta daraja sifuri kwa matokeo kidato cha nne.
Ikumbukwe katika ziara yake ya siku tatu aliyoifanya mbunge wa jimbo la Bunda mjini kwa jumla ya shule 16 za sekondari za Bunda mjini ametoa jumla ya magunia 65 ya mahindi na kilo 800 za maharage ikiwa ni kuunga mkono juhudi za wazazi kuchangia chakula cha wanafunzi shuleni ili kuongeza kiwango cha taaluma.
No comments:
Post a Comment